Jumamosi 24 Oktoba 2026 - 17:38
Tamasha la Waislamu Wenye Asili ya Afrika Latangaza Washindi wa Tuzo Zake

Hawza/ Waislamu nchini Uingereza wameendesha tamasha la kutambua na kuenzi huduma na mafanikio ya Waislamu Wenye Asili ya Afrika, wenye ushawishi mkubwa ambapo tuzo za thamani zimetolewa kwa washindi.

Kwa mujibu wa Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, wanachama mashuhuri wa jumuiya za Waislamu Wenye Asili ya Afrika, kutoka maeneo mbalimbali ya Uingereza wameenziwa katika hafla maalumu ya utoaji wa tuzo za kifahari.

Katika mazingira ya kitamaduni na kisiasa ambapo simulizi kuhusu Waislamu Wenye Asili ya Afrika, mara nyingi hupuuzwa au kupunguzwa na kuwasilishwa kwa kutumia mitazamo ya kimfumo na dhana potofu, tamasha la Tuzo za Waislamu Wenye Asili ya Afrika, 2026 limewasilisha simulizi tofauti; simulizi linaloangazia mafanikio, ubunifu, uongozi na huduma kwa jamii.

Hafla hiyo iliyohudhuriwa na watu wengi ilifanyika katika kituo maarufu cha sanaa cha Zafran, kilichopo Stratford, jijini London. Hafla hiyo ilielekeza umakini wa watu kwenye mchango mkubwa unaotolewa na Waislamu Wenye Asili ya Afrika, katika jamii nzima ya Uingereza, huku ikiwaenzi watu binafsi na mashirika ambayo shughuli zao zinachangia kuijenga na kuiendeleza jamii, pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili.

Tuzo yenye heshima kubwa zaidi katika hafla hiyo ilikuwa Tuzo ya Malik al-Shabazz, jina ambalo linajulikana zaidi kama Malcolm X na lenye umuhimu wa pekee wa kihistoria na kitamaduni. Tuzo hiyo ilitolewa kwa Roman Muhammad, mtafiti katika Taasisi ya Aziz na mkufunzi ambaye kazi yake inalenga masuala ya utambulisho, kujiamini na utamaduni wa kitaasisi.

Katika kazi zake, Bw. Muhammad huwasaidia watu binafsi na taasisi kupitia huduma za ushauri, kwa lengo la kujenga mazingira ambayo watu wanajihisi kuwa na uwezo wa kujikwamua, kujiendeleza na kuongoza kwa kuzingatia malengo yenye maana.

Kwa miaka mingi, tukio hili limebadilika na kuwa zaidi ya hafla ya kawaida ya utoaji wa tuzo. Tamasha hilo lilikuwa ukumbusho wa michango ambayo Waislamu Wenye Asili ya Afrika, wanaendelea kuitoa katika jamii nzima ya Uingereza, michango ambayo mara nyingi haipati kutambuliwa kwa kiwango kikubwa na umma.

Marian Abdullah, mkurugenzi na mwanzilishi wa tamasha hilo, alisema: “Kila mwaka, tunajivunia kuwatambulisha zaidi kwenye umma watu binafsi na mashirika ambayo shughuli zao zinainua jamii, zinawatia moyo wengine na kuleta mabadiliko chanya na endelevu, kupitia tamasha hili la kifahari.”

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha